Saratani ya koo la Chakula
Vihatarishi vya kansa ya koo
Ingawa chanzo halisi cha kansa ya koo hakijulikani, mambo yafuatayo yanaweza kusababisha mtu kupata saratani ya koo. Hata hivyo, pamoja na kuwepo vihatarishi hivi, ni vigumu kueleza kwa ufasaha kwa nini mtu au watu fulani wanaweza kupatwa na kansa ya koo na mtu mwingine asipate. Vihatarishi hivi ni
- Umri: Hatari ya kupata saratani ya koo huongezeka zaidi kwa watu walio na umri wa miaka 65 na kuendelea. Hata hivyo saratani ya koo aina ya adenocarcinoma inaweza kutokea hata kwa wanawake walio na umri kuanzia miaka 40 na kuendelea.
- Jinsia: Tafiti nyingi zimeonesha kuwa wanaume wana uwezekano wa kupata saratani ya koo mara tatu zaidi ya wanawake.
- Uvutaji sigara: Wavutaji sigara wapo katika hatari ya kupata saratani ya koo ukilinganisha na wasio wavutaji.
- Unywaji pombe wa kupindukia: Unywaji wa pombe kwa kiasi cha chupa tatu na zaidi kwa siku unamuweka mnywaji katika hatari ya kupata saratani ya koo ikilinganishwa na mtu asiyekunywa kabisa pombe. Aidha wanywaji wa kupindukia ambao pia ni wavutaji sigara wana hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya koo ikilinganishwa na wanywaji wa pombe wasio wavutaji sigara. Kwa maneno mengine, unywaji pombe pamoja na uvutaji sigara hufanya kazi kwa pamoja kuongeza uwezekano wa mtu kupata saratani ya koo.
- Lishe: Kuna mjadala kuhusu mchango wa aina fulani za vyakula katika kusababisha saratani ya koo. Wakati watafiti wengine wanasema ulaji wa matunda na mboga mboga husaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya koo, watafiti wengine wanapinga kuhusu suala hilo.
- Unene kupindukia : Unene wa kupitiliza huongeza uwezekano wa kupata saratani ya koo aina ya adenocarcinoma.
- Matatizo ya tumbo: Matatizo sugu katika tumbo yanayosababisha tindikali kurudi kwenye koo (acid reflux) kutoka tumboni husababisha madhara katika seli za koo na hatimaye kupelekea saratani ya koo kwa baadhi ya watu.
- Tatizo sugu la kucheua kwa tindikali: Iwapo tatizo la tindikali kucheuliwa kwenye koo litaendelea kwa muda mrefu mpaka kuwa sugu, sehemu ya chini ya koo yaweza kuathiriwa na kusababisha hali ijulikanayo kitaalamu kama Barrett esophagus. Hali hii huongeza uwezekano wa kutokea kwa saratani ya koo.
Dalili za saratani ya koo
Mgonjwa mwenye saratani ya koo katika hatua za awali anaweza asioneshe dalili zozote zile. Hata hivyo, kadiri saratani inavyozidi kukua na kuenea, mgonjwa anaweza kuwa na dalili zifuatazo:
- Chakula kukwama kwenye koo
- Siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate
- Maumivu wakati wa kumeza chakula hasa chakula kigumu
- Maumivu kwenye kifua au mgongoni
- Kupungua uzito
- Kiungulia
- Sauti ya mkwaruzo au kikohozi kikavu cha zaidi ya wiki mbili
Hata hivyo ifahamike kuwa dalili hizi zinaweza kutokea pia kwa baadhi ya magonjwa mengine tofauti na saratani ya koo. Hivyo ni vizuri kumuona daktari kwa uchunguzi zaidi.
Maoni
Chapisha Maoni