Saratani ya Matiti
Saratani ni aina ya ugonjwa unaosababisha ukuaji wa seli za mwili kubadilika na kukua bila mpangilio maalum.
Saratani ya matiti hutokea kwenye titi ambalo kwa kawaida lina sehemu ya kutengeneza maziwa ijulikanayo kama lobules na aina fulani ya mishipa inayounganisha hizi lobules na chuchu za titi. Sehemu kubwa iliyobakia ya matiti inajumuisha mafuta na tishu ambazo kitaalamu tunazoita connective and lymphatic tissue. Saratani ya matiti inayotokea kwenye lobules huitwa lobular carcinoma na ile inayotokea kwenye ducts huitwa ductal carcinoma.
Baadhi ya saratani ya matiti zinaongeza ukubwa kutokana na kuwa na vishikizi aina ya receptors zinazojulikana kama estrogen receptors kwenye seli zao ambazo husababisha ukuaji wa saratani ya matiti.
Kuna wanawake wengine wana viashiria vya asili vinajulikana kama HER2 positive breast cancer ambacho husaidia seli kuongezeka, kugawanyika na kujirekebisha pale zinapoharibika. Kiashiria hiki kinaaminika ndicho kinachosababisha wanawake hawa kuwa na saratani ya matiti yenye madhara zaidi na kuwa na uwezekano mkubwa wa kujirudia kwa saratani baada ya tiba tofauti na wale ambao hawana kiashiria hiki cha HRE2.
Vihatarishi vya Saratani
Kuna mambo kadhaa ambayo yameonekana kuwa na uhusiano, ama wa moja kwa moja au kwa kupitia vitu vingine, wa kusababisha saratani ya matiti, au kumfanya mtu au kundi la watu kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huu kuliko wengine. Mambo hayo ni pamoja na
- Jinsia: Ingawa, saratani ya matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.
- Umri: Uwezekano wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu. Kadiri umri wa mtu unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa mkubwa. Wanawake walio na umri wa kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa (mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45.
- Uasili wa mtu (ethnicity): Saratani ya matiti hutokea zaidi kwa wanawake wazungu kuliko wanawake wa kiafrika au wenye asili ya afrika (weusi).
- Uzazi: Wanawake ambao hawajazaa au kunyonyesha wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti. Wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 nao pia wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.
- Historia ya ugonjwa huu katika familia: Wanawake walio katika familia zenye historia ya ugonjwa huu wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale ambao hawana historia ya ugonjwa huu katika familia zao. Kwa mwanamke aliye na ndugu (mama, dada au mtoto) ambaye aliwahi kupata saratani hii kabla ya umri wa miaka 50, uwezekano wa mwanamke huyu kupata ugonjwa huu ni mara mbili ya yule ambaye hana historia hii.
- Umri wa kuvunja ungo: Wanawake wanaovunja ungo (kupata hedhi) kabla ya umri wa miaka 12 wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
- Kuacha kupata hedhi: Kwa kawaida wanawake huacha kupata hedhi wafikapo miaka 45, hali ambayo kitaalamu hujulikana kama menopause. Wanawake wanaochelewa kuacha kupata hedhi, kwa mfano wale wanaoendelea kupata hedhi wakiwa na zaidi ya miaka 45, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya matiti.
- Historia ya saratani ya matiti: Wanawake ambao wamewahi kupata ugonjwa huu kwenye titi la upande mmoja hapo kabla, wana uwezekano mkubwa wa kupata tena saratani kwenye titi la upande mwingine hapo siku za usoni.
- Ulaji wa vyakula venye mafuta mengi: Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake wanaopendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
- Kuongezeka uzito: Tafiti nyingine zimeonesha kuwa, wanawake wanene wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti ukilinganisha na wale wa uzito mdogo au wa kati.
- Uvutaji sigara: Kuna matokeo yenye kukinzana kuhusu uhusiano wa uvutaji sigara na hatari ya kupata saratani ya matiti. Wakati baadhi ya tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya uvutaji sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti, tafiti nyingine zinaonesha majibu yenye kutofautiana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na saratani ya matiti. Hata hivyo, kwa ujumla, wanawake wanaojizuia kuvuta sigara wanakuwa na afya njema zaidi kuliko wale wanaovuta sigara.
- Unywaji pombe: Imeonekana kuwa wanawake wanaokunywa pombe zaidi ya chupa moja kwa siku wana uwezekano wa kupata saratani ya matiti kwa asilimia zaidi ya ishirini.
- Historia ya tiba ya mionzi: Wanawake ambao wamewahi kupata tiba ya mionzi hususani wakati wa ukuaji wa matiti, wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Hali hii husababishwa na ukweli kuwa mojawapo ya madhara ya mionzi ni kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya aina yoyote.
- Matumizi ya dawa za kupanga uzazi: Kuna ushahidi kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya vidonge vya kupanga uzazi.
- Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni mwilini: Kwa wale wanaotumia tiba ya homoni inayojulikana kama hormone replacement therapy, kwa sababu nyingine yeyote ile, au wale wenye kiwango kikubwa cha homoni kama vile oestrogen na progesterone mwilini mwao wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua saratani ya matiti.
- Kuwa na matiti makubwa: Wanawake wenye matiti makubwa (dense breast tissue) wana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya matiti. Hali hii hutokana na ukweli kuwa wakati mwingine ni vigumu sana kwa madaktari kutambua kama wana saratani au la kutokana na ukubwa wa matiti yao.
Dalili za Saratani ya Matiti
Dalili ya awali inayoweza kutambulisha saratani ya matiti ni kuwepo kwa uvimbe kwenye titi ambao huwa na hali tofauti na sehemu nyingine za titi. Hata hivyo, si kila uvimbe kwenye titi unaashiria uwepo wa saratani ya matiti. Uvimbe huu huwa mgumu, unaochezacheza kwenye titi, ambapo wakati mwingine unaweza kuwa na maumivu makali au kusiwe na maumivu yeyote. Uvimbe huu huwepo zaidi ya mzunguko mmoja wa hedhi kwa wale ambao hawajaacha kupata hedhi.
Dalili nyingine ni pamoja na
Kuwepo kwa uvimbe kwenye sehemu za kwapa
- Sehemu ya titi kuingia ndani inayoashiria uvimbe usioonekana au usioweza kuhisiwa
- Mabadiliko kwenye chuchu, kama vile chuchu kuzama ndani au kuwa na nundu ndogo ndogo, chuchu kuwasha, kuhisi kama kuchoma, kidonda kwenye chuchu au chuchu kuwa na kovu ambalo huashiria saratani ya sehemu hiyo
- Kubadilika kwa umbo la titi, ngozi ya titi kuwa kama ganda la chungwa (peu de orange), ngozi kuwa na rangi nyekundu, na kuongezeka kwa joto kwenye titi. Dalili hizi huashiria kusambaa kwa saratani mwilini.
- Dalili nyingine ni chuchu kutoa maji yasiyo ya kawaida ambayo hayana rangi. Aidha wakati mwingine, chuchu hutokwa damu au majimaji yenye rangi nyingine tofauti.
Tiba ya saratani ya matiti
Upasuaji
Lengo kuu la upasuaji ni kuondoa saratani kwenye titi pamoja na tezi (lymph nodes). Zipo aina kadhaa za upasuaji unaoweza kufanywa kwenye titi lililogundulika kuwa na saratani. Aina hizo ni pamoja na
- Lumpectomy: Huu ni upasuaji unaofanywa kuondoa sehemu ya saratani pamoja na sehemu ya titi ambayo haijaathirika kwa saratani. Hii hufuatiwa na tiba ya mionzi (radiotherapy) kwa muda wa kati ya wiki 6 au 7. Mgonjwa anayefanyiwa aina hii ya upasuaji anakuwa na uwezekano wa kuishi muda mrefu sawa na anayefanyiwa upasuaji wa kuondoa titi lote lililoathirika.
- Simple ama Total mastectomy: Ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika kwa ugonjwa wa saratani.
- Radical mastectomy: Aina hii ya upasuaji uhusisha uondoaji wa titi lote na kundi la tezi liloathirika kwa saratani, pamoja na misuli ya sehemu za kifua (chest wall muscles). Hata hivyo, upasuaji wa aina hii ni nadra sana kutumika siku hizi.
- Modified radical mastectomy: Ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika pamoja na kundi lote la tezi (lymph nodes) chini ya mkono (axilla) bila kuhusisha uondoaji wa misuli ya kifua.
Kwa ujumla, lumpectomy na mastectomy, zote zinahusisha uondoaji wa kundi la tezi ambalo lipo karibu na uvimbe wa saratani (regional lymph nodes).
Tiba ya mionzi
Mionzi inaweza kutumika kuharibu seli za saratani zilizobaki kwenye matiti, kifua (chest wall), au/na eneo la chini ya mkono mara baada ya upasuaji kufanyika. Mionzi pia inaweza kutumika kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani kabla ya kufanyika kwa upasuaji.
Tiba ya saratani kwa njia ya dawa (Systemic therapy)
Tiba ya aina hii inahusisha matumizi ya kemikali maalum za kutibu saratani (chemotherapy) pamoja na matumizi ya homoni (hormonal therapy).
Tiba kwa kutumia homoni (Adjuvant hormonal therapy) hutumika ili kuua seli za saratani ambazo hazikugundulika hapo awali na ambazo yawezekana zimesambaa sehemu nyingine za mwili. Tiba hii hutolewa baada ya kufanyika kwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani.
Aina hii ya tiba hutegemea na ukubwa wa uvimbe, matokeo ya vipimo vya kimaabara vya saratani (histological results), na iwapo saratani imesambaa hadi kwenye tezi za kwenye kwapa la mgonjwa ama la. Tiba hii pia yaweza kutolewa kwa mgonjwa ambaye saratani imeshasambaa mwilini kwake kwa muda mrefu, na ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji.
Dalili za saratani kusambaa mwilini
- Maumivu ya mifupa
- Maumivu kwenye titi
- Vidonda kwenye ngozi
- Kuvimba mkono karibu na eneo la saratani
- Kupungua uzito.

Maoni
Chapisha Maoni