Ugonjwa wa Kifua kikuu (TB)

Ugonjwa wa kifua kikuu ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea sana kwa watu masikini duniani (Disease of poverty). Magonjwa mengine katika jamii ya disease of poverty ni malaria na Ukimwi (AIDS). Ugonjwa wa kifua kikuu huathiri asilimia 98 ya watu katika nchi zinazoendelea, ukimwi asilimia 95 na malaria asilimia 90.

Ugonjwa wa kifua kikuu, husababishwa na bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis. Kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama Mycobacteria tuberculosis (husababisha kifua kikuu), Mycobacteria leprae (husababisha ugonjwa wa ukoma), Mycobacteria bovis (huathiri ngombe na binadamu), Mycobacteria afrikanum na kadhalika.
Ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu, mifupa, mfumo wa mzunguko wa damu, ngozi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system.
Kuna aina kuu tatu za ugonjwa wa kifua kikuu
  • Kifua kikuu kinachosababisha madhara (Active tuberculosis) – Hutokea pale ambapo bakteria waliopo mwilini wapo hai na kinga ya mwili imeshindwa kuwadhibiti hawa bakteria wasisababishe madhara. Watu hawa wanaweza kumuambukiza mtu yoyote kifua kikuu kwa njia ya kuvuta pumzi kama watakohoa, kutema mate, kupiga chafya, kupiga kelele iwapo watafanya vitendo hivi karibu na watu wasio na ugonjwa huu.
  • Ugonjwa usiosababisha madhara (Inactive tuberculosis) – Kwa kitaalamu pia unaitwa latent TB. Hapa inaamaanisha ya kwamba kinga ya mwili imeweza kuwadhibiti bakteria na kuwafanya kushindwa kusababisha madhara. Mtu mwenye latent TB, hana dalili za ugonjwa huu, hajisikii mgonjwa na hawezi kuambukiza mtu mwingine ugonjwa wa kifua kikuu. Aina hii inaweza kujirudia baadae na kuathri sehemu ya juu ya mapafu na hivyo kusababisha kikohozi cha kawaida ambacho baadae huongezeka na kusababisha kikohozi cha damu au makohozi, homa, kupungua hamu ya kula, kupungua uzito bila sababu ya msingi na kutokwa jasho kwa wingi kuliko kawaida wakati wa usiku.
Ugonjwa uliosambaa Mwilini (Milliary tuberculosis) – Hii hutokea pale ambapo kinga ya mwili imepungua na kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu kuenea kupitia damu hadi sehemu nyingine za mwili kama mifupa, mishipa ya fahamu, ngozi, figo, kibofu cha mkojo, ngozi ya moyo (pericadium), mfumo wa uzazi, viunganishi vya mifupa (joints) na lymphatic system. Husababisha homa, kupungua hamu ya kula, kuchoka na kupungua uzito.   

Vihatarishi vya ugonjwa wa kifua kikuu

Vihatarishi vya ugonjwa huu ni kama ifuatavyo
  • Kuzeeka
  • Unywaji pombe kupindukia
  • Kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kambi za jeshi nk.
  • Magonjwa yanayoathiri kinga ya mwili kama Kisukari nk.
  • Wafanyakazi wa huduma ya afya
  • Ugonjwa wa HIV
  • Utapia mlo
  • Umaskini au hali duni ya kipato
  • Kuishi kwenye nyumba za jamii mfano nyumba za wazee
  • Wale wasio na makazi
  • Baadhi ya dawa – Dawa za ugonjwa wa maumivu ya mifupa (athritis)
  • Wasafiri au watalii kutoka nchi zilizo na idadi kubwa ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Dalili na viashiria vya ugonjwa wa kifua kikuu

  • Kukohoa zaidi ya wiki 2-3 na kuongezeka kutoa makohozi
  • Kukohoa damu
  • Homa
  • Kupungua hamu ya kula
  • Kupungua uzito kwa asilimia 10 ya mwili.
  • Kutokwa na jasho kwa wingi wakati wa usiku
  • Uchovu
  • Maumivu makali ya kichwa
  • Maumivu ya kifua
Kupumua kwa shidashida

Tiba ya kifua kikuu

Tiba ya kifua kikuu inahusiha matumizi ya dawa za kifua kikuu kwa muda wa miezi sita au tisa. Dawa hizi zinahusisha matumizi ya miezi 2 ya kwanza ya dawa aina ya isoniazid, rifampicin, pyrazinamide, na matumizi ya miezi 4 ya isoniazid, rifampicin na ethambutol au streptomycin. Dawa hizi hutolewa chini ya uangalizi yaani mgonjwa anakunywa chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya (Directly Observe Treatment, short course). Tiba ya ugonjwa wa kifua kikuu inatolewa bure nchini kote Tanzania.
Upasuaji unaweza kufanyika kwenye mapafu kama dawa zimeshindwa kutibu kifua kikuu.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu

  • Chanjo ya ugonjwa wa kifua kikuu ipo na inasaidia kukinga TB (BCG Vaccine) na imeleta mafinikio katika kukabiliana na kifua kikuu. Kawaida hutolewa kwa watoto baada ya kuzaliwa.
  • Kuziba pua na mdomo kwa kitambaa (mask) ili kujikinga na kifua kikuu.
  • Kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha kinga ya mwili.
  • Kupata usingizi wa kutosha.
  • Kwenda hospitali kufanya vipimo mara kwa mara. Inashauriwa kufanya kipimo cha ngozi angalau mara moja kwa mwaka.
  • Kuimarisha kinga ya mwili kwa kula vyakula venye virutubisho vyote muhimu kwa afya bora.
  • Kutumia dawa aina ya isoniazid (INH) kwa wale walio kwenye hatari ya kuambukizwa kifua kikuu.
  • Shirika la afya duniani (WHO) linapendekeza wagonjwa wa ukimwi (HIV) ambao wana Latent TB wapewe dawa ya isoniazid (INH) kama kinga dhidhi ya kifua kikuu kila inapohitajika.
  • Kuepuka mikusanyiko au mrundikano wa watu kama vile kwenye mabweni, kambi za jeshi, baa nk
  • Kuishi kwenye nyumba ambayo ina mfumo mzuri wa kuingiza na kutoa hewa yaani iwe na madirisha makubwa na ya kutosha.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Saratani ya koo la Chakula

Tiba mbadala ya vidonda vya Tumbo

Homa ya Malale (African Sleeping sickness)